Tags

Tuliza moyo kipenzi, moyo wako na upoe,
Upunguzie wasi wasi, hofu yote iondoe,
Penzi letu sio haba, huzuni yako itoe,
Tuliza moyo kipenzi, Penzi letu limefika!

Tuliza moyo kipenzi, ni mbali tumetoka,
Tumeyaona mabaya, lakini penzi likaponea,
Na mengine yenye miba, maumivu kutuletea,
Tuliza moyo kipenzi, Penzi letu limefika!

Tuliza moyo kipenzi, ya zamani yamepita,
Uchungu tusije beba, mwishoye tukaja juta,
Tusikijaze kibaba, kwa yale yaliyopita,
Tuliza moyo kipenzi, Penzi letu limefika!

Tuliza moyo kipenzi, wenye kusema waseme,
Wanajifanya wajuaji, sumu yao waiteme,
Yarabi twalia haki, hawa ni mpaka wajute,
Tuliza moyo kipenzi, Penzi letu limefika!

Tuliza moyo kipenzi, penzi letu likomae,
Wa mbinguni yeye Baba, dua zetu apokee,
Atujaze mara saba, penzi letu lendelee,
Tuliza moyo kipenzi, Penzi letu limefika!

Tuliza moyo kipenzi, la moyoni nimesema,
Busu langu liwe tiba, likutakialo mema,
Moyoni ninakubeba, u mawazoni daima,
Tuliza moyo kipenzi, Penzi letu limefika!

Advertisements